Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Burundi, Mhe.Gervais Ndirakobuca amesema ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam ndio uliosaidia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa nchi hiyo. Mhe. Ndirakobisca amesema hayo alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza utendaji kazi wa bandari hiyo, Pamoja na kujionea maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanyika bandarini hapo. Ikumbukwe Bandari ya Dar es Salaam ilifanya maboresho makubwa ya miundombinu yake ikiwemo ujenzi wa magati yake kuanzia RoRo hadi gati namba 7. Mbali ya magati hayo, Bandari hiyo pia ilifanikiwa kuongeza kina cha maji magatini hadi kufikia urefu wa mita 14.5 na kuongeza kina cha sehemu ya kugeuzia meli na lango la kuingia bandarini. “Tumefurahishwa sana na kazi inafanyika hapa bandarini, na pia tunapongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha miundombinu ya Bandari hii muhimu kwetu” amesema. Amesema kwamba, kimsingi Bandari hii imesaidia sana kukuza uchumi wa nchi yetu ya Burundi. tunaomba MUNGU aendelee kuimarisha ushirikiano mwema uliopo kati ya Burundi na Tanzania. Aidha Waziri Mkuu Ndirakobuca ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuendelea kuboresha ulinzi katika mipaka ya Tanzania na Burundi na hivyo kuleta utulivu, kupunguza uharifu na kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika. Wakitoa maelezo ya awali kuhusu utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Tanzania, Mhe Prof. Makame Mbarawa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa walimhakikishia Waziri Mkuu huyo kuwa Serikali itaendelea kufanya maboresho makubwa ya miundombinu katika Bandari zake ili kuongeza ufanisi. Mwisho