BODI YA WAKURUGENZI WA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI TANZANIA YATEMBELEA BANDARI YA MTWARA

 

  • MKANDARASI WA UJENZI WA GATI AHIMIZIWA KUMALIZA KAZI KWA WAKATI

Bodi ya wakurugenzi ikiongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Ignas Rubaratuka imetembelea Bandari ya Mtwara tarehe 12-13.09.2019 kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na ujenzi wa gati moja unaoendelea.

Bodi hiyo ilipata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa gati ambapo wameishauri Menejimenti ihakikishe kwamba inasimamia kwa karibu mradi huo ili uweze kumalizika kwa wakati.

Mradi huo uliwekwa jiwe la msingi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 04 Machi, 2017 ambapo ulitarajiwa kukamilika tarehe 31 Agosti, 2019 lakini umeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo kuwepo kwa udongo usiofaa ambao ulihitajika kuchimbwa kabla ya kuanza ujenzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko ameieleza Bodi kwamba Menejimenti imejipanga vizuri kusimamia mradi huo kwa karibu na wataendelea kushirikiana na Mhandisi mshauri wa Mradi huo ili kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu aliishukuru Bodi ya Wakurugenzi kwa kuridhia na kutoa punguzo maalum (Concessionary Tariff) kwa Kiwanda cha Saruji Dangote ili kiweze kutumia Bandari ya Mtwara kusafirisha saruji yake, usafirishaji huo unategemewa kuanza hivi karibuni. Pia Mkurugenzi Mkuu aliitaka Menejimenti ya Bandari ya Mtwara kujiandaa kuhudumia shehena hiyo kwa wakati na kwa kasi inayotakiwa.

Mkurugenzi Mkuu pia aliitaka Menejimenti ya Bandari ya Mtwara kujiandaa kuhudumia shehena ya Makaa ya Mawe ambayo yanatarajiwa kuanza kusafirishwa kwa kupitia Bandari ya Mtwara.

Nae Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mhandisi Juma Kijavara aliishukuru Bodi kwa kuidhinisha ‘Concessionary Tariff’ kwa ajili ya kusafirisha Saruji na akawahakikishia kwamba tayari Bandari ya Mtwara imejipanga kikamilifu kuhudumia shehena hizo zinazotarajiwa kupitia Bandarini hapo kwa wakati.

 

Katika Picha ni Matukio mbalimbali kuhusiana na Ziara ya Bodi:

PIC 5

PIC 1

PIC 2

PIC 4

PIC 6

PIC 7PIC 8

PIC 9