Na Enock Bwigane
Ujumbe wa Maofisa wa Forodha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Forodha na Ushuru wa bidhaa Bw. René Kalala Masimango, umeipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania - TPA kwa kuweka mikakati madhubuti ya ujenzi na uimarishwaji wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Mkoa wa Pwani.
Bw. Masimango anayesimamia Majimbo ya Haut Katanga, Lualaba, Tanganyika na Lomami ametoa pongezi hizo tarehe 05 Mei,2023 alipotembelea Bandari Kavu ya Kwala ili kujionea utayari wa Bandari hiyo katika kutoa huduma.
“Tunawapongeza kwa kazi nzuri. Majimbo ninayoyasimamia, Jimbo la Haut Katanga linapokea asilimia 80 ya Shehena ya DRC inayopitia Bandari ya Dar es Salaam, hivyo ni muhimu sana kwetu kufika hapa katika Bandari Kavu ya Kwala ili kujionea utayari wale kwa ajili ya kuhudumia shehena zetu”, amesema Bw. Masimango.
Naye Balozi wa Tanzania nchini DRC Mhe. Said Juma Mshana amesema lengo la ziara hii ya Kibiashara ni kuona utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam na hii ya Kwala ili kuimarisha Biashara Kati ya Tanzania na DRC.
“Tupo hapa kurahisisha Biashara, uwekezaji na kutanua masoko kati ya nchi hizi mbili za Tanzania na DRC na hii yote ni katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi,” amesema Mhe. Balozi Mshana.
Ujumbe huo ukiwa katika Bandari Kavu ya Kwala, pia umetembelea na kukagua eneo la Hekta 10 lililotengwa na Serikali kwa ajili ya kuhudumia Shehena ya mzigo wa DRC unaopita Katika Bandari ya Dar es Salaam.
Ujumbe huo na umepewa maelezo ya kina kuhusu mradi huo na Meneja miliki wa TPA Bw. Alexander Ndibalema ambaye amesema kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa Bandari hiyo kutapunguza msongamano Katika Bandari ya Dar es Salaam kwa Asilimia 30 na kuongeza mapato ya Serikali kupitia huduma zinazotolewa Katika Bandari.
Kukamilika kwa Bandari kavu hiyo ya Kwala iliyofikia Asilimia 95 ya ujenzi wake, ni matokeo chanya ya uongozi madhubuti ya Serikali ya awamu ya sita ambayo imewezesha Shilingi Bilioni 83.247 kwa ajili ya kujenga na kuendeleza Bandari hiyo, ikuhusisha pia Ujenzi wa Barabara ya Zege yenye urefu wa kilometa 15.5 kutoka Barabara ya Morogoro kuingia na kutoka Bandarini hapo pamoja na miundombinu ya reli mchepuko yenye urefu wa kilometa 1.3 ambayo pia inayoingia na kutoka katika Bandari hiyo.
Mwisho