Maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, yameiwezesha Bandari hiyo kuongeza uwezo na sasa inauwezo wa kuhudumia meli kubwa na za kisasa zenye urefu hadi kufikia mita 305.
Akizungumzia uwezo wa Bandari hiyo, mara baada kukamilika kwa ukarabati wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bwana Plasduce Mbossa amesema kwa sasa Bandari hiyo ipo tayari kwa ajili ya kuhudumia meli za aina hiyo kwa ufanisi.
Kabla ya ukarabati huo, Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye urefu wa mita zisizozidi 250 na ikitokea ikiingiza meli kubwa zaidi basi hazidi mita 300.
“Tumeongeza kina cha maji na kuimarisha zaidi magati yetu ambapo kwasasa yana uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi na zenye urefu mkubwa kwa ufanisi mkubwa,” amesema Mbossa. Serikali kupitia TPA imefanya maboresho makubwa ya magati ya Bandari hiyo kwa kuyafanya kuwa ya kisasa zaidi pamoja na kuongeza kina kwenye magati hayo, hadi kufikia urefu wa mita 14.5 kwenye gati namba 1 – 7.
Mbali ya kuboreshwa kwa magati hayo, eneo la kugeuzia meli pia limeongezwa upana hadi kufikia mita 520 ili kuwezesha meli za kubwa zaidi kuingia Bandarini kwa urahisi.
Sambamba na maboresho hayo, lango kuu la kuingia Bandarini pia limechimbwa na kuwa na urefu wa kina cha mita 15.5 pamoja na upana wa mita 200. Mbali ya maboresho hayo, Bandari hiyo pia imejenga gati mpya na ya kisasa ya kushushia magari (Ro-Ro) na hivyo kuifanya Bandari hiyo kuwa ya kisasa zaidi na ufanisi wake kuongezeka maradufu.
Bandari ya Dar es Salaam ni moja kati ya Bandari mama zinazoendeshwa na kumilikiwa na TPA (Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania). Bandari nyingine ni pamoja na Bandari za Tanga na Mtwara na zile zilizo katika maziwa ya Nyasa, Victoria na Tanganyika.
Muonekano wa Magati katika Bandari ya Dar es Salaam
Meli maalum ya magari ikishusha magari katika gati jipya ya kushushia magari (RoRo)
Muonekano wa gati mpya ya kushushia magari ikiwa na shehena ya magari
Moja ya Meli Kubwa za Makasha ikiingia katika Bandari ya Dar es Salaam