Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa (kulia) akipokea moja ya tuzo hizo toka kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Dkt Doto Biteko Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeendelea kung’ara kwa mara ya tatu mfululizo kwa kutwaa Tuzo ya Mwajili Bora wa mwaka katika Sekta ya Umma kwa mwaka 2024. Wakati wa hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, ilishuhudiwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa akipokea Tuzo hizo toka kwa mgeni rasmi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko, ambaye alimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango. Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw Plasduce Mbossa (katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Mbarikiwa Masinga (kulia), pamoja na Meneja Rasimali Watu, Bw. Mussa Mzenga mara baada ya kukabidhiwa tuzo za Mwajli Bora wa mwaka Sekta ya Umma, Tuzo ya Mwajili Bora Mzawa, Tuzo ya Mshindi wa Tatu wa Jumla Sekta Zote, Tuzo ya Wanaofanya Vizuri Zaidi na Tuzo ya Mwanachama wa Muda Mrefu wa ATE. Haikuishia hapo, TPA ilitangazwa tena na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kuwa imetwaa Tuzo nyingine nne, ikiwemo Tuzo ya Mwajiri Bora Mzawa (Local Employer Award), ambayo iliiweka Mamlaka hiyo kwenye nafasi ya mshindi wa kwanza. Aidha, TPA pia ilitwaa Tuzo ya mshindi wa tatu wa Jumla Sekta Zote. Tuzo nyingine ni ya Taasisi zinazofanya Vizuri Zaidi (Club of Best Perfomers) na Tuzo ya mwisho ni ya kuwa Mwanachama wa ATE kwa Kudumu Mrefu. Akikabidhi tuzo hizo za umahili kwa uongozi wa TPA, Dkt. Biteko, ameipongeza Menejimenti na Wafanyakazi kwa ushindi huo na kuitaka TPA kuendeleza juhudi zilizofanya ishinde tuzo hizo kwa mara tatu mfululizo. Dkt. Biteko amesema ni jambo la Fahari kubwa kuona taasisi ya kitaifa ya kiuchumi na kimkakati ikipata mafaniko haya na kueleza furaha yake kwa utendaji wa TPA ambao umetambuliwa na ATE pasipo upendeleo wowote. “TPA siyo tu inafanya vizuri kiuchumi, bali pia imeonyesha kwamba ni mwajiri wa kupigiwa mfano na wengine hapa nchini, amesema Dkt. Biteko na kuongeza kwamba taasisi nyingine kuiga mfano huu.” Tuzo hizi hutolewa kila mwaka na ATE kwa waajiri kutoka Sekta za Umma na binafsi ambao wameonyesha utendaji bora na ubunifu katika mwaka husika. Ushindi wa TPA ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuboresha ustawi wa wafanyakazi, kuboresha mazingira ya kazi, na kuendelea kuchangia maendeleo ya Sekta ya Bandari nchini. Kwa mara nyingine, TPA imeonyesha kuwa ni mwajiri wa mfano, si tu katika sekta ya umma bali pia kwa jumla katika sekta zote nchini. Pia katika nyakati tofauti, ndani ya mwaka huu, TPA imeshinda tuzo ya mshindi wa tatu kwa taasisi za umma kwa utoaji huduma bora. Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa mkutano wa siku tatu wa Kikao Kazi kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini hivi karibuni. TPA ni miongoni mwa mashirika yaliyoshiriki katika mkutano huo ambapo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan aliikabidhi Tuzo hiyo kwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Dkt Elinami Minja ambaye aliongozana na Mkurugenzi Mkuu, Plasduce Mbossa. Siri nyuma ya tuzo hizi ni uwekezaji katika kuboresha mazingira bora ya wafanyakazi ndani ya Mamlaka hiyo ambapo wafanyakazi wake, mbali na kupata stahiki zao kwa wakati, wamekuwa wakifaidi mambo mbalimbali, ikiwamo huduma bora za Bima ya Afya, motisha, upandishaji vyeo, mafunzo kwa wafanyakazi, likizo, ushirikishwaji katika maamuzi yanayowahusu na michezo. Mwisho