KIKAO CHA WADAU NA WATEJA

Wateja na Wadau wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Nchini Uganda, wameipongeza TPA kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari zake na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Pongezi hizo wamezitoa mwishoni mwa juma lililopita Jijiji Kampala,
katika tukio lililoandaliwa na Ofisi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa lengo la kuwashukuru kwa kuendelea kuiamini TPA na kuendelea kuchagua kusafirisha shehena kupitia
Bandari zake.
Wateja na Wadau hao pia wametoa maoni yenye lengo la kuboresha zaidi huduma za TPA, kuimarisha ushirikiano na Wateja pamoja na Wadau wake huku wakionesha kufurahishwa na mipango mipya ya kujenga uwezo kwa Mashirika ya Grindrod Logistics Africa na Shirika la Reli la Uganda (URC), Mashirika yanatoa huduma za usafiri kwa njia ya Reli na Maji hususani Ziwa Victoria.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Uganda Mhe.Meje Jenerali Paul Kisesa Simuli, amendelea kuwahakikishia mazingira Rafiki ya kuendelea kufanya Biashara kati ya Nchi hizi mbili hasa kutokana na kuendelea kuongezeka kwa ufanisi katika utoaji huduma katika Bandari zote za TPA. Amesema Ufanisi wa Bandari uliopo sasa unaotokana na Maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika Bandari kupitia TPA, ni faida kubwa katika ukuaji wa Uchumi na Biashara kati ya Nchi hizi mbili pamoja na Uchumi wa kikanda.
Naye Mwakilishi wa TPA Nchini Uganda Bi. Lona Stafford, amewashukuru Wateja na Wadau hao kwa kuendelea kuiamini Mamlaka na kutumia Bandari zake na kusisitiza kuwa TPA itaendelea kuongeza fanisi zaidi katika utoaji wa huduma zake.