Select your language

Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekutana na ujumbe kutoka Chama cha Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Business Congolese Internationale – BCI), katika kikao kilicholenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuongeza matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam na wafanyabiashara wa Kongo. Kikao hicho kimefanyika Septemba 4, 2026 katika Makao Makuu ya TPA, Bandari Tower, jijini Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa kutoa salamu za ukaribisho, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Dkt. Baraka Mdima, amesema shehena kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuongezeka, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuendelea kuboresha huduma na miundombinu ya bandari. 

Dkt. Mdima amesema Serikali kupitia TPA inaendelea kutekeleza jitihada mbalimbali za kuboresha miundombinu na huduma za bandari kwa lengo la kuhakikisha biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaendelea kukua. ''Biashara ya mteja ikikua, na Bandari inakua. Hivyo, jitihada zote tunazofanya katika kuboresha miundombinu na huduma zinalenga kuhakikisha tunakuwa na mazingira bora zaidi kwa wafanyabiashara na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam,” amesema Dkt. Mdima. Ameeleza kuwa ujenzi wa Bandari za Karema na Kigoma ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na kukuza fursa za biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (BCI), Bw. Sumaili K. Edouard, amesema wafanyabiashara wa Kongo wanaiona TPA kama mdau muhimu katika kukuza biashara, akieleza kuwa ushirikiano uliopo umewezesha changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara kushughulikiwa kwa haraka. 

“Wafanyabiashara wa Kongo ni wadau wa TPA na tunaiona TPA kama baba. Changamoto yoyote inapojitokeza, tunapata ushirikiano na inatatuliwa kwa haraka ili kuhakikisha biashara inaendelea kukua,” amesema Bw. Edouard. Ameongeza kuwa wafanyabiashara wa Kongo wanaendelea kuona Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango muhimu la biashara na wanatarajia ushirikiano kati ya BCI na TPA kuendelea kuimarika kwa manufaa ya wafanyabiashara wa mataifa hayo mawili. Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za TPA za kuimarisha ushirikiano na wadau wa biashara kutoka nchi zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam, hususan katika ukanda wa Afrika ya Kati, 
kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma, kukuza biashara na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda huo.

Get In Touch

For any inquiries or support, contact us 24/7
0800-110032
P.O Box 9184 Dar es salaam
dg@ports.go.tz
255 22 2130390

News & Updates DRC

WAFANYA BIASHARA KONGO KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA TPA

25 September 2026

Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekutana na ujumbe kutoka Chama cha Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Business Congolese Internationale – BCI), katika kikao kilicholenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na...
  Tell Me More
TPA YAPONGEZWA NA MJUMBE WA BODI YA CRDB KWA JUHUDI ZA KUPANUA...

01 July 2025

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Bw. Charles Carley, ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa juhudi madhubuti za kupanua wigo wa soko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),...
  Tell Me More