BANDARI KAVU YA KWALA: MLANGO MPYA WA UFANISI WA BIASHARA TANZANIA

Serikali ya Tanzania, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imewekeza katika ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala, mradi wa kimkakati unaolenga kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya kuwa kitovu bora cha biashara kwa nchi jirani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Machi 16, 2025, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati wa ziara yake ya kikazi katika eneo la Bandari Kavu ya Kwala amesema bandari hiyo iliyopo Vigwaza, Kibaha, mkoani Pwani, ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya msongamano wa mizigo bandarini.
Ameeleza kuwa moja ya faida kubwa ya Bandari Kavu ya Kwala ni kupunguza muda wa kushughulikia mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuhifadhi makontena na shehena kubwa ya bidhaa Kwala, ufanisi wa bandari kuu utaongezeka, hivyo wateja kuhudumiwa kwa haraka zaidi.
“Hii itapunguza gharama za ucheleweshaji wa mizigo na kuimarisha mazingira bora zaidi ya biashara na uwekezaji nchini.”
Msigwa amesema bandari hiyo inatarajiwa kuhudumia makasha 823 kwa siku, yakiwemo yanayokwenda nchi jirani. Hii inamaanisha kuwa kwa mwaka itahudumia hadi makasha 300,395, sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam.
Aidha, amesema Serikali imewekeza katika miundombinu muhimu ili kuhakikisha ufanisi wa bandari hiyo, ikiwemo ujenzi wa reli ya mchepuko inayounganisha Kwala na Shirika la Reli Tanzania (TRC), barabara za zege, na mtandao wa umeme wa uhakika.
“Kupitia reli, mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam itaweza kusafirishwa moja kwa moja hadi Kwala, hatua itakayopunguza idadi ya malori barabarani, msongamano, ajali zisizo za lazima na kuokoa barabara zetu,” amesema Msigwa.
Mbali na hayo, Msigwa ameeleza kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu ndani ya eneo la mradi imekamilika kwa asilimia 80.
“Shughuli hizo zinahusisha na Mtandao wa barabara za zege zinazoweza kubeba malori ya mizigo, Jengo la kituo cha kupambana na moto, Jengo la utawala litakalohifadhi ofisi za mashirika ya serikali na watoa huduma za kitaalamu, Mfumo wa maji ya mvua, Mtandao wa umeme na maji safi, Hifadhi za viwanda zenye jumla ya mita za mraba 26,000 na Lango kuu na malazi ya wafanyakazi.”
Kadhalika Msigwa amesema bandari hiyo itakapokamilika, itakuwa na viwanda vikubwa na vya kati 200 pamoja na viwanda vidogo 300 vinavyohusika na Usindikaji wa vyakula, Utengenezaji wa vifaa, Viwanda vya dawa, Vifaa vya ujenzi, Usindikaji wa viatu na nguo, pamoja na Viwanda vya kemikali.
Kwa upande wa Kongani ya viwanda ya SINO-TAN, Msigwa amesema kuwa kongani hiyo itaongeza ajira kwa Watanzania ambapo inatarajiwa kutoa zaidi ya ajira za moja kwa moja 100,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 500,000. Mradi huu unajengwa kwa awamu tano.
Amesema hadi sasa, viwanda vitatu tayari vimeanza uzalishaji, vingine vitatu vipo katika hatua za mwisho za kufunga mitambo, na viwanda vinne vinatarajiwa kuanza ufungaji wa mitambo ifikapo mwisho wa Aprili 2025.
Mwisho