BANDARI YA DAR ES SALAAM NA WADAU WAFANYA KIKAO KWA AJILI YAKUONGEZA UFANISI
Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus Abed, tarehe 23 Januari, 2026, amekutana na wadau wa bandari kujadili masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za kibandari za kila siku, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuhakikisha malengo ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yanafikiwa.
Kikao hicho cha siku moja, ambacho hufanyika kila mwezi, huwakutanisha Menejimenti ya Bandari ya Dar es Salaam na wadau wake wakuu, ambapo hukaa meza moja kujadiliana kwa kina masuala yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma za kibandari, hatua inayochangia kuongeza ufanisi katika uhudumiaji wa shehena na kurahisisha biashara.
Katika kikao hicho, wadau walipata fursa ya kubadilishana mawazo, kutoa maoni na mapendekezo juu ya namna ya kuimarisha uratibu wa shughuli za bandari, kuondoa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku, pamoja na kuboresha ushirikiano kati ya taasisi zinazohusika na mnyororo wa usafirishaji na biashara.
Baadhi ya wadau waliohudhuria kikao hicho ni Waendeshaji wa Bandari DP World Dar es Salaam Limited na Tanzania East Africa Gateway Terminal (TEAGTL), Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Vyombo vya Usalama, Chama cha Mawakala wa Meli Tanzania (TASAA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Menejimenti ya Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kusisitiza umuhimu wa mikutano hiyo ya mara kwa mara kama jukwaa la kujenga ushirikiano, kuongeza uwazi, na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha ufanisi wa bandari kwa manufaa ya taifa na wadau wa biashara kwa ujumla.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"