Select your language

Bandari ya Mtwara imeendelea kupokea wageni mbalimbali ambapo tarehe 16 Aprili, 2026 imepokea ugeni kutoka Kampuni ya Equinor ya nchini Norway wakiongozwa na mwakilishi wao Bw. Noel Cox wakiambatana na mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw. Asiad Mrutu, wamefanya ziara ya kutembelea wadau mbalimbali watakaotoa huduma wakati wa utekelezaji wa mradi wa usindikaji gesi asilia (LNG) unaotarajiwa kufanyika katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.

 

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kutathmini na kujiridhisha kuhusu utayari pamoja na uwezo wa Bandari ya Mtwara katika kuhudumia mizigo mbalimbali itakayohitajika katika utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati mara utakapoanza.

 

Katika ziara hiyo, wageni walipata fursa ya kuelezwa kuhusu maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Mtwara ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa miundombinu ya kupakia na kushusha mizigo, kuongezeka kwa ufanisi wa huduma, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uendeshaji wa shughuli za Bandari. Maboresho hayo yameifanya Bandari ya Mtwara kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuhudumia mizigo ya aina mbalimbali kwa ufanisi na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya miradi mikubwa ya kimataifa. Hali hiyo imechochea utayari wa Bandari katika kuhudumia shughuli za mradi mara utakapoanza.

 

Aidha, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw. Mtunze M. Sudi aliwahakikishia wageni hao kuwa Bandari ipo tayari kuhudumia mizigo yao wakati wowote watakapohitaji huduma hiyo. Alisisitiza kuwa uongozi wa Bandari umejipanga kuhakikisha utoaji wa huduma bora za haraka na zenye viwango vya juu ili kusaidia kufanikisha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya nchi.