Select your language

Baraza la Wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara limefanya kikao chake cha 39 tarehe 23 Februari, 2026 katika Ukumbi wa Klabu ya Bandari.

 

Kikao hicho kiliongozwa na Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Mtunze M. Sudi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo ambapo wajumbe walijadili masuala mbalimbali yanayohusu utendaji kazi, ustawi wa wafanyakazi, kuimarisha nidhamu ya kazi pamoja na kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza tija na ufanisi wa Bandari.

 

Aidha, Baraza hilo lilijadili kwa kina suala la uboreshaji wa miundombinu ya Bandari ambapo imesisitiza umuhimu wa kuimarisha magati, kuboresha maeneo ya kuhifadhia mizigo, kuboresha miundombinu ya TEHAMA kwa ajili ya kurahisisha mifumo ya uendeshaji pamoja na kuboresha barabara za ndani na vifaa vya kushughulikia shehena ili kuongeza kasi na usalama katika utoaji huduma.

 

Baraza lilielekeza juhudi zaidi zifanyike katika kuvutia uwekezaji na kuimarisha matengenezo endelevu ya miundombinu iliyopo ili Bandari iweze kuhudumia meli na shehena kwa viwango vya Kimataifa.

 

Baraza lilipongeza juhudi za Menejimenti na wafanyakazi kwa ushirikiano unaoendelea kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma. Aidha, msisitizo mwingine umetolewa kuhusu umuhimu wa uwajibikaji, mawasiliano ya wazi na mshikamano kazini kama msingi wa mafanikio endelevu.

 

Mwisho, Baraza limeazimia kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maazimio yote yaliyopitishwa katika kikao hicho ili kuhakikisha yanatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi unaotarajiwa

.