BODI YA TPA YATEMBELEA BANDARI YA TANGA
Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo IGP Mstaafu Mhe. Balozi Ernest Mangu, imetembelea Bandari ya Tanga kwa lengo la kujionea hali ya Utendaji katika bandari hiyo.
Bodi hiyo ilipokelewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu Mha. Dkt. Baraka Mdima kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mbosa, na kupokea taarifa ya utendaji kazi wa Bandari ya Tanga.
Akiongea katika ziara hiyo Mhe. Balozi Mangu, amesema maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali katika Bandari nchini ikiwemo Bandari ya Tanga, yataleta manufaa makubwa kiuchumi na kubadili maisha ya Watanzania na kuhudumia pamoja na nchi jirani.
Aidha Bodi hiyo imeiagiza Menejimenti ya TPA kuendelea na mikakati yake ya kutwaa maeneo yaliyopo karibu na Bandari ya Tanga ili kukabiliana na uhaba wa nafasi ya kuhifadhia shehena ya mizigo ambayo imekuwa inaongezeka mwaka hadi mwaka katika bandari hiyo.
Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Bandari, Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega amesema, kwa kipindi cha miezi sita ya mwaka wa fedha 2025/2026 imevuka malengo katika kuhudumia meli, shehena na ukusanyaji wa mapato. Mafanikio hayo yametokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Bodi hiyo pia ilikutana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani, ofisini kwake, ambaye alitoa pongezi kwa Bandari ya Tanga kwa jinsi inavyoshirikiana na serikali ya Mkoa wa Tanga na kuwa na utendaji bora wenye kuvuka malengo katika kuhudumia meli, shehena ya mizigo na ukusanyaji wa mapato.
Katika ziara hiyo, Bodi ya Wakurugenzi wa TPA ilitembelea Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi la EACOP katika eneo la Chongoleani.



EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"