DG AMEKUTANA NA UJUMBE WA JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA YA UBELGIJI

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, tarehe 26 Novemba 2024, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Ubelgiji, Wawekezaji, na Wafanyakazi wa Bandari ya Antwerp.
Ujumbe huo umeongozwa na Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Mhe. Peter Huyghebaert, pamoja na Balozi wa Tanzania katika Ufalme wa Ubelgiji na Jumuiya ya Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga ambapo umetembelea Makao Makuu ya TPA katika Jengo la One Stop Centre, Jijini Dar es Salaam, na kukutana na Menejimenti ya TPA.
Katika mazungumzo yao, waligusia ushirikiano kati ya TPA na Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji katika maboresho ya huduma za kibandari, kulingana na mkataba wa ushirikiano uliopo kati ya TPA na Bandari hiyo. Mazungumzo hayo yalilenga kutoa ushauri elekezi wa kufanikisha mabadiliko chanya ya huduma za kibandari nchini pamoja na kuimarisha ushirikiano wa karibu na jumuiya hiyo.
Aidha, mazungumzo hayo yaligusia nia njema ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maboresho ya Bandari nchini ambapo Bw. Mbossa aliuelezea ujumbe huo kuhusu fursa zilizopo za uwekezaji katika Bandari zote nchini.