DOWUTA BANDARI YA DAR ES SALAAM YACHAGUA VIONGOZI WAKE
Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA) Tawi la Bandari ya Dar es Salaam wamemchagua Bw. Mashaka Karume kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, huku Bw. Eliakimu Maluli akishinda nafasi ya Katibu katika Uchaguzi Mkuu wa DOWUTA uliofanyika tarehe 3 Februari 2026 katika viwanja vya Zimamoto na Usalama Bandari ya Dar es Salaam.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliokuwa sambamba na uchaguzi wa viongozi, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed G. Abed, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, aliipongeza DOWUTA kwa kudumisha utulivu na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi, hali inayochangia kuboreshwa kwa maslahi yao na kuongeza ufanisi kazini.
Bw. Abed alisema kuwa utulivu na moyo wa kujituma wa wafanyakazi, kwa kiasi kikubwa, umechagizwa na mchango wa DOWUTA, hali iliyopelekea kuongezeka kwa ufanisi wa kazi bandarini. Alieleza kuwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka wa fedha 2025/2026, Bandari ya Dar es Salaam imehudumia tani milioni 16.7, ongezeko la tani milioni 3.9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Aidha, alisema kuwa kwa kasi hiyo ya utendaji, Bandari ya Dar es Salaam inatarajiwa kuhudumia zaidi ya tani milioni 32 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2025/2026, kiwango kinachozidi lengo la tani milioni 27.7, mafanikio aliyoyataja kuwa ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Menejimenti na DOWUTA.
Katika nafasi nyingine za uongozi, Bi. Sharifa Yahya amechaguliwa kuwa Mweka Hazina, Bw. Shabani Godigodi akishinda nafasi ya Mwakilishi wa Watu Wenye Uhitaji Maalum, huku Bw. David Mtambazi na Bi. Tunu Masenga wakishinda nafasi za Uwakilishi wa Vijana Wanaume na Wanawake mtawalia.
Kwa upande wa Wajumbe Wanawake waliochaguliwa ni Bi. Dainess J. Binemukama, Bi. Theopista W. Millinga, Bi. Chema Y. Mwaduga, Tatu Mandao na Dr. Bertha O. Mushi, huku wajumbe wa idara mbalimbali wakichaguliwa kuwakilisha sekta zao ikiwemo Uhandisi, Utekelezaji, Ulinzi na Zimamoto, Marini, Bandari Ndogo, Rasilimali Watu na Utawala pamoja na Usaidizi wa Biashara, Ugavi, Fedha na Mapato.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"