Select your language

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Serikali kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala, ikieleza kuwa mradi huo ni suluhisho muhimu la changamoto ya msongamano wa malori katika Bandari ya Dar es Salaam na maeneo ya Jiji kwa ujumla.

 

Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Bandari kavu ya Kwala iliyopo Mkoa wa Pwani, Machi 19, 2026, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso( Mb), amesema kukamilika kwa mradi huo kunaongeza ufanisi wa upakuaji na usafirishaji wa Shehena.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa ( Mb) amesema mpango uliopo ni kuiunganisha Bandari Kavu ya Kwala na reli ya SGR na MGR pamoja na bandari nyingine, hatua itakayoongeza ufanisi wa usafirishaji na kupunguza gharama za biashara.

 

Aliongeza kuwa mradi huo utaenda sambamba na maendeleo ya Eneo Maalumu la Kiuchumi (SEZ) ili kuifanya Kwala kuwa kitovu cha usafirishaji (Regional Logistics Hub).

 

Aidha, ameihakikishia Kamati kuwa maoni, ushauri na maelekezo yote yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo yatafanyiwa kazi kwa lengo la kuongeza zaidi ufanisi wa huduma bandarini na kuimarisha mchango wa sekta ya bandari katika kukuza uchumi wa Taifa.

 

Naye , Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mha. Dkt. Baraka Mdima kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, amesema mafanikio ya sekta ya bandari yanatokana na ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi, akisisitiza kuwa maboresho yanayoendelea yataongeza ushindani, kuvutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.