KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU IMERIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA TPA KATIKA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Serikali kwa mabadiliko makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam na kuleta tija na ufanisi mkubwa katika kuhudumia Shehena.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Selemani Kakoso ( Mb) tarehe 18 Machi 2025, baada ya Kamati kutembelea na kukagua mradi wa maboresho wa Bandari ya Dar es Salaam.
“ Tunaipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa na kiwango kikubwa cha mabadiliko kilichofanyika. Tumeona hakuna kuchelewa wala kukwama kwa huduma ya shehena, hakika mafanikio ni makubwa na mapato yameongezeka sana, hakika uwekezaji umelipa.” Amesema Mhe. Kakoso.
Mhe. Kakoso pia ametoa Rai kwa Menejimenti ya TPA kuhakikisha inatenga maeneo makubwa na ya kutosha kwa ajili ya faida ya baadae kwa matumizi ya Bandari kwani mtaji mkubwa kwa maendeleo ya Bandari ni ardhi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile( Mb) ameishukuru Kamati kwa ziara yao iliyowawezesha kuona kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika maboresho makubwa ya miundombinu kwenye Bandari ya Dar es Salaam huku akiihakikishia kamati hiyo kuwa maoni, ushauri na maelekezo waliyoyatoa yatafanyiwa kazi.
Mapema akisoma taarifa ya maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam kwa kamati kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka Mdima,amesema maboresho ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam yameleta tija na ufanisi mkubwa katika kuhudumia Shehena Bandarini hapo na hivyo kuchagiza ongezeko la makusanyo ya mapato ya Nchi.
“ Mapato yaliyokusanywa na TPA kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024, yamefikia Shilingi Trilioni 1.4 na kulingana na taarifa mbalimbali za kiuchumi, mchango wa sekta ya Bandari katika mapato yanayotokana na ushuru wa forodha, yameongezeka kwa asilimia 18, kutoka wastani wa Shilingi Bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia wastani wa Shilingi Trilioni 1.” Amesema Dkt. Mdima.
Pia Dkt. Mdima amesema TPA inathamini na ushirikiano inaoupata kutoka Serikalini, hususani kutoka katika Kamati hiyo na kusisitiza kuwa ushirikiano zaidi unahitajika ili Mamlaka iweze kutekeleza mipango yake inayolenga kuboresha miundombinu na tija katika Bandari zote nchini, ili kuwa chachu ya maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.