KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEWZAJI WA MITAJI YA UMMA (PIC) YAKAGUA MABORESHO YA UPANUZI WA BANDARI YA MWANZA KASKAZINI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imemuelekeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Menejimenti yake kuendelea kumsimamia ipasavyo Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maboresho na upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini ili aweze kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa kiwango kulingana na thamani ya fedha.
Akizungumza Machi 21, 2025 Jijini Mwanza baada ya kutembelea na kukagua mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Augustine Vuma (Mb),amesema kukamilika kwa wakati kwa mradi huo ni hatua muhimu katika kuboresha hali ya usafiri na usafirishaji ndani ya Ziwa Viktoria.
“ Kwa ujumla Sekta ya Bandari Mhe. Rais ametoa fedha nyingi sana na kwa hili tunampongeza sana kwa uamuzi wake huu maana tunaona miradi mingi ya maboresho na ujenzi wa bandari pamoja na ukarabati na ujenzi wa Meli. Kwa ujumla TPA mnafanya kazi nzuri na tunawapongeza kwa mradi huu mzuri na wa kimkakati, muhimu ni usimamizi makini ili mapato yaongezeke na tija ionekane.” Amesema Mhe.Vuma
Pia ameiagiza TPA kuhakikisha inaendeleza ushirikiano na Sekta Binafsi ili kuongeza ufanisi zaidi katika Bandari na kuendelea kuimarisha maeneo ya pembezoni kupitia Bandari.
Akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Mhe. Balozi na IGP Mstaafu Ernest Mangu, ameishukuru Kamati kwa ziara yao iliyowawezesha kuona mradi wa maboresho na upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini, huku akiihakikishia kamati hiyo kuwa maoni, ushauri na maelekezo waliyoyatoa yatafanyiwa kazi.
Mapema akisoma taarifa ya mradi wa maboresho na upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini mbele ya kamati kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mbossa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka Mdima,amesema kukamilika kwa maboresho na upanuzi wa Bandari hiyo kutaenda sambamba na mabadiliko ya kisasa ya Teknolojia katika kuendesha Bandari na kutoa huduma za kiwango cha kisasa zaidi ikiwa ni pamoja na kuongeza tija na ufanisi mkubwa katika kuhudumia Shehena.
Mradi wa maboresho na upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini unagharimu shilingi Bilioni 18.6, ikiwa ni jitihada za Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) katika kuboresha hali ya usafiri na usafirishaji ndani ya Ziwa Viktoria.