KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) AKAGUA MWARI WA USANIFU NA UJENZI WA BANDARI MPYA YA MBAMBA BAY

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ameiagiza Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Bandari mpya wa Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma unakamikika kwa wakati na kwa ubora.
Akizungumza tarehe 05 Aprili,2025 baada ya kutembelea na kukagua mradi huo mkubwa na wa kimkakati, Mhe. Balozi Nchimbi amesema kukamilika kwa Bandari ya Mbamba Bay, kutaimarisha zaidi Biashara katika ukanda wa mikoa ya kusini na nchi jirani za Malawi na Msumbuji.“
“ Mradi huu ni muhimu na faraja kubwa kwa wana Nyasa na unasubiriwa kukamilika kwake. TPA hakikisheni mnausimamia kwa nguvu zenu zote kwani ni Jambo Jema kwa maendeleo ya nchi yetu.” Amesema Mhe. Balozi Nchimbi.
Mhe.Balozi Nchimbi pia ameipongeza Menejimenti ya TPA kwa kuusimamia vyema Mradi huo muhimu na wa kimkakati ambao anasema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatoa umuhimu wa pekee katika kukamilika kwake.
Mapema akitoa maelezo ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mbossa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka Mdima, amesema mradi huo utakaojengwa kwa miezi 24, unatarajia kukamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.
Amesema ujenzi wa Bandari ukikamilika utafungua biashara kati ya Tanzania na nchi za Zambia, Malawi na Msumbiji na kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar-es-Salaam, kuongeza ufanisi katika Bandari ya Mtwara na kuimarisha kiuchumi ushoroba wa kusini.
Mradi huu unajengwa katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 49,700 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 81 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 26 na unatarajia kukamilika katika kipindi cha miezi 24.
Jiwe la msingi la usanifu na Ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay, liliwekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Septemba 25, 2024.