Select your language

Ujumbe kutoka Jamhuri ya Malawi ukijumuisha maofisa kutoka Shirika la Reli la Malawi na Idara ya Huduma za Reli, taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi ya Malawi, tarehe 24 Juni 2026 umetembelea Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kupata uelewa wa kina kuhusu shughuli za bandari pamoja na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutekelezwa bandarini hapo.Ujumbe huo ulipokelewa na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed G. 
Abed, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa.Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Abed aliueleza ujumbe huo kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa katika kuboresha miundombinu, mifumo ya uendeshaji na utoaji huduma bandarini, hatua ambazo zimeendelea kuongeza ufanisi wa bandari na kuimarisha ushindani wake katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.Aidha, alieleza kuwa Malawi ni miongoni mwa nchi jirani zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa usafirishaji wa shehena zake za kuagiza na kusafirisha nje, huku ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi ukiendelea kuimarika kupitia sekta ya uchukuzi na usafirishaji.Kwa mujibu wa takwimu za TPA, shehena ya Malawi iliyopitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kutoka tani 579,796 katika mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia tani 675,200 katika mwaka wa fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 16.5.Ujumbe huo umeeleza kuridhishwa na maendeleo na maboresho yanayoendelea kufanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, huku ukisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Malawi na Tanzania katika sekta ya uchukuzi wa reli na bandari kwa manufaa ya biashara na uchumi wa nchi hizo mbili.