Select your language

Dar es Salaam — Maboresho makubwa ya miundombinu ya bandari nchini, hususan Bandari ya Dar es Salaam, yameendelea kuleta matokeo chanya kwa kuongeza mapato ya Serikali, ufanisi wa utoaji huduma na kuvutia idadi kubwa ya watumiaji kutoka nchi jirani, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiongoza kwa kutumia huduma za bandari hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam kama sehemu ya kuelezea mafanikio ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amesema maboresho hayo yamechochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango kuu la biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Bw. Msigwa amesema uwekezaji uliofanywa umeongeza ufanisi katika ubebaji na usafirishaji wa shehena kwenda nchi jirani, hali iliyosaidia kupunguza muda wa meli kukaa bandarini na kuongeza ushindani wa bandari za Tanzania kikanda na kimataifa.

Ameeleza kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati kuboresha bandari, kwa lengo la kukuza biashara, kufungua fursa za uwekezaji na kuhakikisha bandari zinachangia kikamilifu ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka wa fedha 2024/2025, bandari za Tanzania zimehudumia shehena kubwa kwa nchi jirani ambapo DRC imeongoza kwa tani 5,995,293, ikifuatiwa na Zambia tani 3,510,706, Rwanda tani 1,724,370, Malawi tani 675,200, Burundi tani 425,774, Uganda tani 185,625, Zimbabwe tani 61,306 na nchi nyingine tani 38,512.

Katika kuimarisha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, TPA ilisaini mikataba ya upangishaji na uendeshaji na kampuni za DP World MEA FZE na Adani International Ports Holdings Pte Limited, ambazo zilianzisha kampuni za DP World Dar es Salaam Limited na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Bw. Msigwa amesema hadi kufikia Juni 2025, DP World imewekeza takribani Shilingi bilioni 214.2 katika ununuzi wa mitambo mipya, matengenezo ya mitambo ya TPA, usanifu wa mifumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ukarabati wa karakana na uboreshaji wa maeneo ya kuhifadhi shehena.

Kwa upande wake, TEAGTL inaendelea na uwekezaji wa Shilingi bilioni 410.4 unaohusisha ukarabati wa miundombinu, maboresho ya gati namba 8 hadi 11, ununuzi wa mitambo mipya na usimikaji wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA.

Uwekezaji huo umeleta mafanikio makubwa, ikiwemo ongezeko la shehena hadi tani milioni 27.7 katika mwaka wa fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2025, bandari ilihudumia tani milioni 16.7, ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.

Aidha, muda wa kuhudumia meli za makasha umepungua kutoka wastani wa siku 30 hadi siku 6, hatua iliyopunguza gharama za biashara. Uwekezaji huo pia umechangia kutoa ajira 764 za moja kwa moja hadi Juni 2025, pamoja na maelfu ya ajira zisizo za moja kwa moja kwa madereva, mawakala wa forodha na wafanyakazi wa kutwa.

Bw. Msigwa ameongeza kuwa ushirikiano na wawekezaji hao umeiwezesha TPA kupunguza gharama za uendeshaji kwa wastani wa asilimia 57 na kuongeza uwiano wa faida kutoka asilimia 66 hadi 78. Hali hiyo imeongeza makusanyo ya kodi ya forodha hadi Shilingi trilioni 12.33 katika mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 17.

Kwa upande wa miradi inayoendelea, TPA inatekeleza ujenzi wa gati na matanki 15 ya kuhifadhi mafuta yenye uwezo wa lita 378,000 kwa wakati mmoja, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 35. Pia kuna mradi wa uboreshaji wa Gati la Malindi lenye urefu wa mita 500, pamoja na miradi ya uboreshaji wa Gati Na. 8–11 na upembuzi yakinifu wa Gati Na. 12–15.

Kadhalika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea na mradi wa ujenzi wa reli ndani ya Bandari ya Dar es Salaam (MGR, SGR na TAZARA), ambao ukikamilika utaongeza uwezo wa kuhudumia hadi TEUs 480,000 kwa mwaka na kuongeza usafirishaji wa mizigo kwa reli kutoka asilimia 2 hadi asilimia 12.

Kwa ujumla, maboresho hayo yameifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa kichocheo kikuu cha biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi wa Tanzania na nchi jirani.

Maboresho mengine pia yamefanyika katika bandari mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa bandari ya Kisiwa Mgao Mtwara, maalum kwa ajili ya kuhudumia shehena ya mzigo mchafu (Dirty Cargo) kama vile Makaa ya Mawe na Saruji.

Amesema Mkandarasi anaendelea na utekelezaji wa mradi huu ambao hadi sasa umefikia asilimia 18 ya utekelezaji.

Hali kadhalika ujenzi wa upanuzi wa bandari ya Bukoba, ambao ulihusisha ujenzi wa gati ya kuhudumia shehena ya magari (RO-RO) na meli, kizuia upepo (wind breaker), ujenzi wa eneo la maegesho ya magari pamoja na ujenzi wa jengo la abira. Bandari nyingine ni pamoja na  upanuzi wa bandari ya Kemondo uliokamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa bandari ya Mwanza North ( asilimia 80), huku kazi kama hizo zikiendelea katika bandari nyingine ikiwemo bandari za Kigoma, Tanga na Mbamba Bay.

Mwisho.