Select your language

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaendelea kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya ExpoBeton 2026 yanayoendelea mjini Kalemie, Jimbo la Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC ) kuanzia Mei 27–30, 2026.Maonesho hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali kutoka nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika wakiwemo makampuni ya madini, wafanyabiashara, wasafirishaji pamoja na taasisi za serikali kwa lengo la kujadili fursa za biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu katika ukanda huo.Katika Maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP (Mstaafu) Balozi Simon Sirro, alishiriki katika jopo la Majadiliano na kuiwakilisha vyema Tanzania katika mijadala muhimu iliyogusia maendeleo ya miundombinu, biashara ya kikanda, maboresho ya bandari za Tanzania, ujenzi wa meli katika Ziwa Tanganyika pamoja na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na DRC. 

Kupitia ushiriki wake, TPA ikiwakilishwa na Afisa Mwakilishi wake katika Jiji la Lubumbashi, jimbo la Haut Katanga Bw. Othman Mkangara, imeendelea kutangaza fursa zinazopatikana katika Bandari za Ziwa Tanganyika na mchango wake katika kurahisisha biashara na usafirishaji kwa nchi za ukanda huo, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa maendeleo ya uchumi wa Afrika Mashariki na Kati.