Select your language

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetwaa Tuzo ya Ushindi wa Kwanza katika Kundi la Uwezeshaji Bora wa Biashara na Uwekezaji, ikiwa ni utambuzi wa mchango wake katika kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji nchini.Tuzo hiyo ilikabidhiwa Julai 3,2026 na Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Shariff Ali Shariff, kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
TPA imeendelea kutekeleza maboresho ya miundombinu ya bandari, kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma na kuimarisha ufanisi wa ushughulikiaji wa mizigo na meli. Maboresho hayo yamechangia kuongeza uwezo wa Bandari za Tanzania katika kuhudumia Shehena, kupunguza muda wa utoaji wa huduma na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Utambuzi huo unathibitisha nafasi ya TPA katika kuchochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi wa taifa kupitia huduma bora za bandari.