Select your language

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kupitia Bandari zake za Ziwa Nyasa inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya Biashara ya Mbeya Expo 2026, yanayofanyika katika Viwanja vya Uhindini, jijini Mbeya.Ushiriki wa TPA katika maonesho hayo yaliyoanza tangu tarehe 20 Mei, 2026 na kuendelea hadi 30 Mei 2026 unalenga kuongeza uelewa kwa wadau mbalimbali kuhusu huduma zinazotolewa na Bandari za Ziwa Nyasa, sambamba na kunadi fursa zilizopo katika sekta ya usafirishaji wa majini kwa wananchi, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo wa Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.Kupitia jukwaa hilo muhimu la kibiashara, TPA inatarajia kunufaika kwa njia kadhaa,  ikiwemo kuongeza ufahamu wa umma kuhusu mchango wa Bandari katika kukuza biashara ya ndani na ya kimataifa, kuimarisha mahusiano na wadau wa sekta ya usafirishaji, pamoja na kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa watumiaji na washirika wa huduma za bandari.Aidha, maonesho hayo yatakuwa fursa muhimu ya kutambulisha zaidi bandari za Ziwa Nyasa kwa wafanyabiashara na wateja wa ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, ambao ni miongoni mwa walengwa wakuu wa huduma hizo.

Kupitia maonesho hayo, TPA inalenga kuonyesha mchango wa bandari hizo katika kurahisisha usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa maeneo ya pembezoni mwa Ziwa hilo.Ushiriki wa TPA pia unatarajiwa kufungua milango ya ushirikiano mpana zaidi na sekta binafsi, taasisi za Serikali na wawekezaji, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha matumizi ya Bandari kama kitovu muhimu cha maendeleo ya kiuchumi.Kaulimbiu ya Mbeya Expo 2026, “Kujenga Uchumi wa Kujitegemea,” inaendana na dhamira ya TPA ya kuhakikisha bandari zinachangia kwa vitendo katika ukuaji wa uchumi kupitia usafirishaji salama, wa uhakika na wenye gharama nafuu kwa wananchi na wafanyabiashara wa Tanzania na nchi jirani.Kwa ujumla, ushiriki wa TPA katika Mbeya Expo 2026 ni hatua muhimu ya kimkakati katika kutangaza fursa za bandari za Ziwa Nyasa, kuongeza uelewa kwa wadau, na kuimarisha nafasi ya TPA katika kuchochea maendeleo ya biashara na uchumi katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.