MATOKEO YA UCHAGUZI WA DOWUTA BANDARI YA TANGA
Wafanyakazi wa Bandari ya Tanga wamemchagua Bw. Aliko Mwakipagala kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA) tawi la Tanga, huku Bw. Iddi Mfaume Bode akichaguliwa kuwa Katibu wa tawi hilo.
Pia katika Mkutano huo wa uchaguzi, Wafanyakazi waliwachagua wawakilishi mbalimbali kuunda Kamati ya Utendaji ya DOWUTA tawi la Bandari ya Tanga.
Aidha akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega, alitoa rai kwa wafanyakazi wa Bandari ya Tanga kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha ufanisi unaendelea kunapatikana katika bandari hiyo.
Akiongea katika Mkutano huo Bw. Mbega amesema, ufanisi unaoonekana katika bandari hiyo ni pamoja na utendajikazi uliotukuka kutoka kwa wafanyakazi hivyo, aliwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili tuendelee kuvuka malengo ya kila mwaka yanayotolewa na serikali.
“Bandari ya Tanga imeendelea kuvutia wadau mbalimbali kutaka kufanyakazi na sisi hii yote ni kutokana na tunavyofanya kazi vizuri hivyo nawaomba tuendelee kuwajibika ipasavyo ili mwisho wa siku tufaidike kwa kujituma kwetu”. Aliongeza Bw. Mbega
Aidha Bw. Mbega aliwahakikishia wafanyazi hao changamoto zote zitaendelea kufanyiwa kazi kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kuendelea kuboresha maslahi.
Katika hatua nyingine Bw. Mbega aliwatakia heri wanachama na wagombea wote waliotia nia katika uchaguzi huo na kuwataka kwenda kusimamia maslahi ya wafanyakazi pamoja na mambo muhimu yaliwekwa kwa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi.
Awali akimkaribisha Meneja huyo, Mwenyekiti wa muda wa DOWUTA Tawi la Tanga aliyekuwa anamaliza muda wake Bw. Aliko Mwakipagala alimhakikishia Bw. Mbega kuwa chama hicho kitaendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi wa bandari ili kuhakikisha malengo katika uhudumiaji wa shehena yanafanikiwa.
Katika kipindi cha kwanza Mwakipagala alishikia nafasi ya Mwenyekiti baada ya aliyekuwa Mwenyekiti Bw. Ali Sankole kustaafu utumishi wake bandarini.



EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"