MIUNDOMBINU YA UCHUKUZI MWAMBAO WA ZIWA TANGANYIKA KUIMARISHWA
Serikali imesema imejipanga kuhakikisha miundombinu ya usafirishaji inaendelea kuboreshwa ili kusaidia ukuaji wa biashara na utoaji huduma katika ukanda wa mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Akizungumza katika Mkutano wa Kamati ya Uongozi ( Steering Committee) kuhusu mapitio ya miradi ya miundombinu ya Usafiri kwa ajili ya kuimarisha Biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tarehe 18 Machi,2026 Mjini Kigoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, amesema kuwa maboresho ya bandari, reli pamoja na usafiri wa majini hususan katika Ziwa Tanganyika yataongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kupunguza gharama za biashara kati ya nchi hizo.
“DRC ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa Bandari za Tanzania, Lengo letu ni kuona ukanda huu unakuwa kitovu cha biashara chenye ushindani mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Hii itasaidia kuvutia uwekezaji na kufungua fursa zaidi za ajira kwa wananchi wetu,” alisema Prof. Kahyarara.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka DRC, Roger Te-Biasu, aliishukuru Tanzania kwa ushirikiano mzuri na kusisitiza kuwa nchi hizo zinaendelea kushirikiana katika miradi ya kimkakati ya miundombinu ili kukuza biashara na uchumi wa kikanda.
Naye Katibu Mtendaji wa wakala wa uwezeshaji wa usafirishaji wa Ushoroba wa kati (CCTTFA), Wakili. Flory Okandju, amewahimiza Wadau wa sekta ya usafirishaji na logistiki kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazojitokeza katika ukanda wa Ziwa Tanganyika ili kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Alibainisha kuwa taasisi hiyo inaendelea kuratibu juhudi za nchi wanachama ikiwemo Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC kwa lengo la kurahisisha biashara na usafirishaji katika ukanda huo.
Katika majadiliano, kamati imepongeza hatua zilizofikiwa katika bandari, reli, barabara na usafiri wa anga, huku ikibainisha haja ya kuharakisha miradi iliyochelewa hususan upande wa DRC.
Mkutano huo umehitimisha kwa makubaliano ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi, kuendeleza ushirikiano wa karibu, na kuhakikisha fursa zilizopo zinatumika kikamilifu ili kukuza biashara na maendeleo ya kiuchumi kati ya Tanzania na DRC.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"