MKURUGENZI MKUU AZUNGUMZA NA WATUMISHI WAPYA WA TPA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, amewataka watumishi wapya wa taasisi hiyo kuweka maslahi ya umma mbele ya maslahi binafsi na kuutumikia umma kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji ili kulinda imani ya wananchi kwa Serikali.
Akizungumza wakati wa kufungua kozi ya awali ya mafunzo kwa watumishi wapya (Induction Course) iliyofanyika Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam, tarehe 2 Februari,2026, Bw. Mbossa amesema Serikali inawatazamia watumishi wa umma kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya ndani ya taasisi zao na katika jamii kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa utumishi wa umma si ajira ya kawaida, bali ni wito wa kulitumikia taifa kwa uaminifu na uzalendo wa dhati, akiwahimiza watumishi wapya kuzingatia maadili ya kazi, kufanya kazi kwa weledi na kujenga utamaduni wa uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Kumbukeni kuwa imani ya wananchi kwa Serikali hujengwa au hubomolewa kupitia mwenendo wa watumishi wake,” alisema Bw. Mbossa, akionya dhidi ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha taswira ya taasisi na utumishi wa umma kwa ujumla.
Aidha, aliwahimiza watumishi wapya kutumia mafunzo waliyoyapata kama msingi wa kujenga taaluma zao, wakizingatia misingi ya uadilifu, weledi na uzalendo, sambamba na kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto badala ya kuwa chanzo cha matatizo.
Akihitimisha hotuba yake, Mkurugenzi Mkuu aliwatakia watumishi wapya mafunzo mema na safari njema katika utumishi wa umma, akisisitiza umuhimu wa kulinda heshima ya taasisi na Taifa kwa ujumla.
Kozi hiyo ya “induction” inalenga kuwaandaa watumishi wapya wa TPA kwa kuwajengea uelewa wa majukumu ya taasisi, misingi ya utumishi wa umma, maadili ya kazi na matarajio ya Serikali katika kuboresha ufanisi wa bandari na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.



EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"