Select your language

Serikali imesisitiza dhamira yake ya kushirikiana na Bandari ya Mtwara ili kuhakikisha mnyororo mzima wa thamani katika usafirishaji wa zao la korosho unatekelezwa kwa ufanisi na mafanikio makubwa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Bandari ya Mtwara, uliofanyika Septemba 29, 2025 mkoani humo, ikiwa ni maandalizi ya msimu wa korosho 2025/2026.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, mwakilishi wake Bw. Emmanuel Mrutu alisema ufanisi wa bandari na utoaji wa huduma bora unategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa karibu kati ya bandari na wadau wake.

Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, alieleza kuwa mkutano huo ni wa umuhimu mkubwa kwani unakutanisha wadau wakuu wanaotumia bandari hiyo, huku ukiwa fursa ya kipekee kwa wateja na wadau kupata mrejesho kuhusu maandalizi ya bandari ya Mtwara katika kuhudumia shehena ya korosho kwa msimu huu wa kilimo.

Aidha, Bw. Nyathi alitumia jukwaa hilo kueleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kuhudumia shehena ya korosho kwenye msimu uliopita, akisisitiza kuwa Bandari ya Mtwara imejipanga vizuri kuhakikisha msimu wa 2025/2026 unakuwa na tija zaidi kwa wakulima na wadau wote wa zao hilo.

Uchaguzi 2025 Logo