Select your language

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (MNEC) Comrade Richard Kasesera,tarehe 3 Februari, 2026 ameongoza ujumbe wa Wanachama wa CCM katika ziara ya kikazi ya kutembelea Bandari ya Mtwara.

Lengo la ziara hiyo ni kujionea maendeleo ya Bandari ya Mtwara baada ya maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kupata taarifa ya utendaji kazi wa Bandari.

Katika ziara hiyo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Kapt. Paul Muchwampaka alieleza masuala mbalimbali ikiwemo mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto kadhaa zinazoikabili Bandari ya Mtwara.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Comrade Kasesera alipongeza utendaji kazi mzuri wa Bandari ya Mtwara ikiwa ni pamoja na uwezo mkubwa wa kuhudumia shehena. Aidha, alieleza kuwa atawasilisha katika ngazi za juu masuala mbalimbali ikiwemo changamoto zilizopo ili zitafutiwe ufumbuzi wa haraka kwa lengo la kuendelea kuimarisha ufanisi na mchango wa Bandari ya Mtwara katika maendeleo ya Taifa.