Select your language

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kusambaza mafuta ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji kikanda na kimataifa.

 

Rais Dkt.Samia amesema hayo wakati alipoweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kusambaza mafuta Kigamboni jijini Dar es Salaam.

 

Mhe.Rais ameitaka Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vya Kimataifa ili kukidhi hitaji la ushindani wa soko la Dunia.

 

Katika hotuba yake ya kumkaribisha Mhe. Rais,Waziri wa Uchukuzi Mhe.Prof .Makame Mbarawa amesema huu ni mradi utakaoongeza uwezo wa bandari katika kuhudumia meli za mafuta na kuifanya Tanzania kuaminika na wadau wa sekta ya usafirishaji wa ndani na Kimataifa.

 

Katika salamu zake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw.Plasduce Mkeli Mbossa amesema siku ya leo inashuhudia jitihada za dhati za Mhe.Rais Samia Suluhu za kuendeleza kuimarisha uwezo na tija za Bandari ya Dar es Salaam kupitia ujenzi wa mradi matanki ya kuhifadhi na kusambaza mafuta.

 

Akizungumzia faida za mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 41, Bw.Mbossa amesema utaongeza ufanisi na kupunguza muda wa meli kusubiri kutoka siku 22 mpaka 7.