Select your language

Bandari ya Dar es Salaam imeandika historia mpya baada ya kupokea meli mpya ya kisasa ya kubeba magari, MV Grande Shanghai, iliyowasili kwa mara ya kwanza ikitokea China katika safari yake ya kwanza. 

Meli hiyo iliyokamilika kujengwa Julai 2025 nchini China,  ina uwezo wa kubeba magari 9,000, ikiwa na urefu wa mita 220 na upana wa mita 38, ambapo katika safari yake ya kwanza imeshusha magari 1,624 yakiwemo malori, mabasi na magari madogo.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya meli hiyo tarehe 21 Septemba 2025, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania( TPA) Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus Abed, amesema ujio wa meli kama hii ni matokeo ya maboresho makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na ushirikishwaji wa sekta binafsi. Alibainisha kuwa uwekezaji katika vifaa vya kisasa umeiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa na za aina yoyote.

Kwa upande wake, Meneja wa Shughuli za Kampuni ya DP World Dar es Salaam, Bw. Elitunu Mallamia, alieleza kuwa ukuaji wa soko na ufanisi wa huduma bandarini ndio vichocheo vikubwa vilivyoleta meli hiyo nchini. 

Ujio wa MV Grande Shanghai unaashiria nafasi ya Tanzania kwenye ramani ya biashara ya kimataifa, na unatarajiwa kuongeza mapato ya serikali, kuvutia wawekezaji na kuifanya Dar es Salaam kuwa kitovu cha usafirishaji wa magari na shehena nyingine Afrika Mashariki.

Uchaguzi 2025 Logo