Select your language

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 3 Machi 2026 ameweka jiwe la msingi la mradi mkubwa wa ujenzi wa Matanki ya Kupokea na Kusambaza Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.

 

Mradi huo wa usanifu na ujenzi wa matanki (Tanks Farm) unatekelezwa na wakandarasi wabia ambao ni China Railway Major Bridge Engineering Group Co. Ltd (CRMBEG) na Wuhuan Engineering Co. Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 678.6 ikijumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

 

Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TPA iliingia mkataba wa usimamizi wa mradi kwa kipindi cha miezi 24 na mshauri elekezi Khatib and Alami Consulting Engineering Offshore S.A.L kwa kushirikiana na Projmors na Anova Consult Company Ltd, kwa thamani ya shilingi bilioni 23.2. Hivyo, kufanya jumla ya thamani ya mradi kufikia shilingi bilioni 701.8.

 

Mradi huu unatarajiwa kuongeza ufanisi wa upokeaji na usambazaji wa mafuta nchini, kupunguza muda wa meli kusubiri bandarini, kupunguza gharama za ucheleweshaji (demurrage) na kuimarisha nafasi ya Bandari ya Dar es Salaam kama kitovu cha biashara ya mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

 

Hatua hii inaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha miundombinu ya kimkakati kwa ajili ya kukuza uchumi wa taifa na kuongeza ushindani wa bandari za Tanzania kimataifa

.