SERIKALI ZA BURUNDI NA YA KONGO (DRC) YAIPONGEZA SERIKALI YA TANZANIA KWA KUIMARISHA BANDARI KAVU YA KWALA

Serikali za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo( DRC) zimetoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mikakati madhubuti ya ujenzi na uimarishwaji wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Mkoani Pwani.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 19 Machi, 2025 na katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi kutoka nchini Burundi Bi. Christine Niragira na Mwakilishi wa Wizara ya Uchukuzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC) Bw. Roger Te- Biasu, baada ya kutembelea Bandari kavu ya Kwala na kukagua maeneo yao yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya kuhudumia Shehena ya mzigo wa Nchi zao unaopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Tunaipongeza Serikali ya Tanzania na tunampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri inayofanyika hapa Kwala na kwa kutupatia eneo hili kwani ni njia ya kurahisisha ufanyaji biashara kati ya Tanzania na Burundi nasi kwa sasa tunaendelea kuliendeleza eneo hili haraka”. Amesema Bi. Niragira.
Serikali ya Tanzania imetenga eneo la Hekta 45 kwa DRC na Hekta 10 kwa Jamhuri ya Burundi katika Bandari Kavu ya Kwala, kwa ajili ya kuhudumia Shehena zao zinazopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
“ Tumefika hapa Kwala kuona eneo tulilopewa na Serikali ya Tanzania na hakika tumeridhika sana kwani ishirikiano uliopo kati ya Nchi hizi zetu mbili ni kwa maendeleo ya pamoja”. Amesema Bw. Roger Te- Biasu.
Ugeni huo umepokelewa na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi Mha. Shomari Shomari kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Uchukuzi, ambaye amesema uwepo wa Bandari kavu ya Kwala ni utekelezaji wa vitendo wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuimarika kwa Bandari kavu hiyo kutafungua Uchumi wa Nchi yetu na kurahisha shughuli za usafirishaji
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA,) Wakili Flory Okandju Okonge, amesema ni faraja kwao kuona nchi saba wanachama aa Ushoroba zinaendelea kunufaika kibiashara na kuendelea kukuza diplomasia ya kiuchumi miongoni mwao kupitia Bandari ya Dar es Salaam na Bandari za Tanzania.
Ujumbe huo umepewa maelezo ya kina kuhusu mradi huo na Meneja Miliki wa TPA Bw. Alexander Ndibalema kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, ambaye amesema kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa Bandari hiyo kutapunguza msongamano Katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza mapato ya Serikali kupitia huduma zinazotolewa Katika Bandari.
Mbali na kujionea maeneo yao hayo pia wamejionea utayari wa Bandari kavu ya Kwala katika kutoa huduma ambayo imekamilika kwa kwa Asilimia 100 ya Ujenzi wake, ikiwa ni matokeo chanya ya uongozi madhubuti wa Serikali ya awamu ya sita ambayo imewezesha Shilingi Bilioni 83.247 kwa ajili ya kujenga na kuendeleza Bandari hiyo, ikuhusisha pia Ujenzi wa Barabara ya zege yenye urefu wa kilometa 15.5 kutoka Barabara ya Morogoro kuingia na kutoka Bandarini hapo pamoja na miundombinu ya reli mchepuko yenye urefu wa kilometa 1.3 ambayo pia inaingia na kutoka katika Bandari hiyo.
Viongozi hao kutoka Nchi za Burundi na DRC pia ni Wajumbe wa Bodi ya Central Corridor inayoendelea na vikao vyake Jijini Dar es Salaam na katika ziara yao hiyo wameongozana na Balozi mdogo wa DRC hapa nchini Mhe. Louis Manzombi Kisombo, Mwakilishi wa Sekta Binafsi wa DRC Mhe. Mudekereza Namegabe, Viongozi kutoka Wizara ya Uchukuzi wakiongozwa na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi Mha. Shomari Shomari aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Naibu Mkurugnzi wa Miundombinu Mha. Christopher Mang’wela na Maafisa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania( TPA).