Select your language

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepongezwa kwa kuweka mikakati ya kuwajengea uwezo Watumishi wanawake ili waweze kufanyakazi na kuleta matokeo chanya kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ,Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha Bi.Sauda Msemo katika hafla ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani iliyoandaliwa na Wanawake watumishi wa TPA na kufanyika katika jengo la Makao Makuu ya TPA jijini Dar es Salaam Machi 15,2025.

Katika salamu zake za ukaribisho Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw.Mbarikiwa Masinga kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA,amewataka Watumishi wanawake kufanyakazi kwa kushirikiana na kupendana bila kuwekeana chuki ili kufikia malengo makubwa ya Taasisi.

Awali akizungumza wakati akiwakaribisha wageni waalikwa katika hafla hiyo, Meneja Rasilimali Watu wa Bandari ya Dar es Salaam Bi.Mwajuma Mkonga amesema walizindua siku ya Wanawake Duniani kwa kupima afya za wafanyakazi na familia zao katika kituo cha afya kilichopo Bandarini na kutoa misaada ya vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 49 na kwamba TPA imekuwa ikifanya hivyo kwa miaka minne mfululizo.

Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani Wanawake watumishi wa TPA walitoa misaada ya vifaa tiba katika hospitali za Wilaya ya Kigamboni vyenye thamani ya shilingi milioni 24 na hospitali ya Rufaa ya Temeke vyenye thamani ya shilingi milioni 25.

Pia katika kuadhimisha siku hiyo wameandaa Tuzo za Mabadiliko Chanya,mwanamke aliyebuni kitu kilicholeta mabadiliko na kuleta tija kwenye Taasisi.

Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani,Watumishi wanawake wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wamebuni shindano la kugombea Tuzo ya Mabadiliko chanya, mchakato uliohitimishwa kwenye halfa iliyofanyika katika ukumbi wa jengo la Makao Makuu wa One Stop Centre jijini Dar es Salaam, Machi 15,2025.

Jaji wa Tuzo hizo Bi.Rosemary Ndesamburo alimtangaza Bi.Lucy Kalinga kuwa mshindi wa tuzo hizo zilizoanza kwa mara ya kwanza mwaka huu huku Bi. Farida Ismaili Hamisi alijinyakulia nafasi ya pili na Bi.Salma Kitwana akipata nafasi ya tatu.