Select your language

Na Mwandishi Wetu

Ili kuendana na malengo ya Uchumi wa Bluu na Bandari ya Kijani (Blue Economy and Green Port), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeeleza hatua madhubuti inazochukua kuhakikisha kuwa shughuli za kibandari haziathiri mazingira.

Akizungumza wakati wa Kongamano na Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STICE), yanayoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dkt. Olivary John kutoka Chuo cha Bandari alieleza kuwa TPA imechukua hatua tano muhimu kudhibiti uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibandari.

Kwa mujibu wa Dkt. Olivary, hatua hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa Sera ya Usimamizi wa Mazingira ya TPA, ambayo inatoa mwongozo wa kulinda na kuhifadhi mazingira katika shughuli za bandari. Hatua nyingine ni uwekaji wa vitunza taka katika maeneo mbalimbali ya bandari ili kuhakikisha taka zinakusanywa na kusimamiwa ipasavyo.

Aidha, TPA imeimarisha juhudi za kudhibiti uzalishaji wa taka, ikiwemo kupunguza taka zinazozalishwa kupitia mbinu endelevu. Pia, mamlaka hiyo inazingatia mfumo wa utunzaji wa mazingira kulingana na kanuni za ISO, kuhakikisha bandari zake zinakidhi viwango vya kimataifa vya mazingira.

Hatua ya tano, kwa mujibu wa Dkt. Olivary, ni utunzaji wa bahari na upunguzaji wa uchafuzi wa mazingira kwa kuondoa taka laini na ngumu katika maeneo ya bahari, ili kuhifadhi usafi na uhai wa viumbe wa majini.

Hatua hizi zinathibitisha dhamira ya TPA katika kufanikisha maendeleo endelevu kupitia ulinzi wa mazingira na kuhakikisha bandari zake zinachangia uchumi wa taifa bila kuathiri mazingira.