TPA YAISHUKURU SERIKALI KWA AJIRA MPYA NDANI YA SIKU 100
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeishukuru Serikali kwa kuijumuisha miongoni mwa taasisi za umma zilizobahatika kupata waajiriwa wapya ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua inayolenga kuimarisha ari, ufanisi na utoaji huduma katika TPA pamoja na Bandari ya Dar es Salaam.
Shukrani hizo zimetolewa , tarehe 23 Februari 2026, na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus Abed, wakati akifungua mafunzo elekezi ya siku moja kwa waajiriwa wapya 95 watakaohudumu katika Bandari ya Dar es Salaam. Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Zimamoto na Usalama, Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Abed amesema kuwa ahadi ya Mhe. Rais ya kuunda ajira mpya ndani ya siku 100 imezaa matunda, ambapo TPA, hususan Bandari ya Dar es Salaam, imepata fursa ya kuongeza watumishi watakaosaidia kuongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi.
Aidha, amewataka waajiriwa hao kufanya kazi kwa weledi, nidhamu na kujituma, wakitambua kuwa wanachangia moja kwa moja katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa pamoja na nchi jirani zinazotegemea huduma za bandari hiyo.
Pia amewapongeza kwa kuaminiwa na kuajiriwa na TPA, akiwahimiza kuwa chachu ya kuwezesha na kufanikisha biashara kupitia lango kuu la biashara la taifa, kwa kuishi na kutenda kama watumishi waliodhamiria kufungua na kukuza uchumi wa nchi.
Mafunzo hayo elekezi yameenda sambamba na mapokezi rasmi ya watumishi hao wapya, watakaopangiwa katika idara na vitengo mbalimbali vya Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha utoaji huduma na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi

.
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"