Select your language

Link: https://www.instagram.com/reel/DS7mMD9iAys/?igsh=bnhpZm4wcXpwa3Fi 

Bandari ya Dar es Salaam imeandika historia mpya baada ya kupokea kwa mara ya kwanza meli kubwa ya kisasa inayoendeshwa kwa nishati safi ya gesi asilia (LNG) iitwayo Höegh Australis, inayomilikiwa na kampuni ya Höegh Autoliners kutoka Norway.

Meli hiyo yenye urefu wa mita 200 imeshusha magari 1,006, na inaashiria ongezeko la imani ya makampuni makubwa ya usafirishaji wa kimataifa kwa uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa wakala wa meli hiyo, Bw. Prosper Setebe kutoka kampuni ya EACS (East African Commercial and Shipping Company), ujio wa Höegh Australis ni matokeo ya maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika bandarini.

“Bandari ya Dar es Salaam sasa ni lango la kimataifa, si la kikanda tu. Maboresho ya miundombinu, matumizi ya teknolojia na huduma za kisasa vimeivutia meli kubwa kama hii kuleta shehena zake hapa,” alisema Bw. Setebe.

Maboresho hayo ni pamoja na:

                       Kuimarika kwa kasi na ufanisi wa kushusha na kupakia mizigo.

                       Uwekezaji kwenye vifaa vya kisasa vya kupakua shehena.

                       Huduma za kidigitali zinazorahisisha uendeshaji wa shughuli za bandari.

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejenga mazingira wezeshi ya kuvutia wawekezaji na kufanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa chaguo la kwanza kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

“Natoa wito kwa wadau wote kuendelea kuitumia Bandari ya Dar es Salaam kwani sasa ni ya kisasa na ina ufanisi mkubwa,” aliongeza Bw. Setebe.

Ujio wa meli ya LNG ni ishara ya Tanzania kujiweka kwenye ramani ya usafirishaji wa kimataifa kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira.