Select your language

Baraza la Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa limeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa juhudi kubwa za kuboresha na kuendeleza bandari nchini, likieleza kuwa maendeleo yanayoonekana katika Bandari ya Mtwara ni ushahidi wa usimamizi madhubuti na uwekezaji wenye tija unaochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la CCM Taifa, Bw. Vuai Ali Vuai, wakati wa ziara ya kikazi ya wajumbe wa Baraza hilo ambao pia ni Wajumbe wa Bodi ya Jitegemee Holdings Company Ltd katika Bandari ya Mtwara tarehe 24 Julai, 2026.
Ziara hiyo ililenga kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika Bandari ya Mtwara, hususan usafirishaji wa makaa ya mawe, pamoja na maendeleo ya miundombinu ya bandari. Wajumbe hao walipata maelezo kuhusu utendaji wa bandari na kutembelea maeneo mbalimbali ya shughuli za kibandari. Akiwasilisha taarifa ya utendaji, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, alisema bandari imeendelea kuhudumia kwa ufanisi zaidi ya tani milioni 1.2 za makaa ya mawe kwa mwaka, huku shehena hiyo ikichangia zaidi ya asilimia 60 ya makusanyo ya mapato ya bandari. Alieleza kuwa maboresho ya miundombinu yameongeza uwezo wa kuhudumia shehena kwa haraka na kupunguza muda wa meli kukaa bandarini hadi wastani wa saa 72.
Wajumbe hao pia walitembelea mradi wa ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao, ambao umefikia asilimia 43 ya utekelezaji. Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa Bandari ya Mtwara kuhudumia shehena chafu (dirty cargo), ikiwemo makaa ya mawe, na kuimarisha nafasi ya bandari hiyo kama lango muhimu la biashara na usafirishaji wa mizigo nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.