Select your language

Wadau wa sekta ya Uchukuzi wanaoshiriki Mkutano wa pili wa Uchukuzi na Usafirishaji - East Africa Cargo Connect Summit Jijini Dar es Salaam, wametakiwa kuutumia Mkutano huo kuwa na majadiliano yenye faida na yenye kuleta maazimio chanya yatakayoleta mchango mkubwa wenye kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za uchukuzi zikiwemo za kibandari.

Kauli hiyo imetolewa tarehe 27 Machi, 2025 na Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA Dkt. George Fasha aliyewakilishwa na Afisa Masoko Mkuu Bi. Fatma Adadi Rajab ambaye amesema majadiliano yenye tija ni muhimu kwani mkutano huo unaonyesha nia ya dhati ya Wadau wa Uchukuzi katika kuiboresha sekta hiyo na kuhakikisha utoaji huduma unaendelea kuwa bora zaidi.

Mkutano huo wa siku moja ni jukwaa la kuwakutanisha pamoja Wadau wa sekta ya uchukuzi kwa njia ya maji, anga, reli na barabara, kujadaliana pamoja changamoto zinazowakabili na utatuzi wake pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji kupitia sekta hiyo na kuikuza zaidi.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imedhamini Mkutano huo ulioshirikisha Wadau wa Uchukuzi kutoka nchi za Afrika Mashariki, Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika ( SADC) na nchi za Afrika magharibi.

Tuzo mbalimbali za umahiri zimetolewa katika Mkutano huo ikiwemo Tuzo ya “The Tanzania Maritime Visionary Leadership Award” iliyotolewa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Bw. Plasduce Mkeli Mbossa kwa kutambua na kuthamini Uongozi wake wenye maono katika sekta ya uchukuzi wa njia ya maji hapa nchini.