TPA YASHIRIKI KIKAO CHA WADAU CHA KUKUSANYA MAONI YA MAREKEBISHO ZA TOZO JIJINI MTWARA
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeshiriki kikao cha siku moja cha wadau wa sekta ya usafiri majini kilichofanyika tarehe 29 Desemba, 2025 mkoani Mtwara, kwa lengo la kukusanya maoni ya umma kuhusu mapendekezo ya marejeo ya tozo za huduma za kibandari kwa bandari za mwambao wa Bahari ya Hindi.
Kikao hicho kiliandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na kuongozwa na Meneja wa Udhibiti wa Huduma za Bandari, Bw. Julius Mitinje, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya kisheria kabla ya kupitisha tozo au viwango vipya vya huduma za kibandari.
Akitoa wasilisho katika kikao hicho, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Josephat Lukindo, amesema mapendekezo haya yana maslahi mapana ya Nchi na lengo lake ni kuboresha ufanisi wa Bandari kwa kuongeza magati, mitambo ya Kisasa ya upakuaji na upakuaji pamoja na maeneo ya kuhifadhia mizigo.
Amefafanua kuwa baadhi ya tozo hizo hazijafanyiwa marekebisho kwa zaidi ya miaka kumi, huku huduma nyingine zikiendelea kutolewa bila kutozwa tozo licha ya kuwa na gharama kubwa za uendeshaji. Aidha, marejeo hayo yanalenga kuziwezesha bandari za Tanzania kutekeleza mipango yake ya uendelezaji wa miundombinu ya bandari, hatua itakayoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kupunguza gharama katika mnyororo wa usafirishaji kupitia bandari nchini.
Akizungumza kando ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dkt. George Fasha, amesema mapendekezo ya marejeo ya tozo yamelenga kuhakikisha bandari za Tanzania zinaendelea kuwa shindani kikanda na kimataifa, zenye ufanisi na zenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya biashara ya kimataifa, huku zikichangia kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ushindani na bandari jirani na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Katika kikao hicho, wadau mbalimbali wa sekta ya bandari na usafiri majini wameipongeza TPA kwa kuwasilisha mapendekezo ya tozo yaliyo himilivu na shindani, wakibainisha kuwa mchakato huo umezingatia uwazi, ushirikishwaji wa wadau na maslahi ya pande zote.
Kwa upande wake, TASAC imeeleza kuwa itaendelea kukusanya na kuchambua maoni ya wadau kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina kabla ya kutoa mapendekezo ya mwisho kuhusu tozo husika. Maoni ya wadau yataendelea kupokelewa kwa maandishi hadi tarehe 30 Desemba, 2025.



EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"