TPA YASHIRIKI MAJADAILIANO YA KUKABIDHANA ARDHI ZAUENDELEZAJI WA MIUNDOMBINU YA BANDARI KAVU KATI YA SERIKALI YA TANZANIA NA KONGO

Serikali ya Tanzania na ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamekamilisha majadiliano ya kukabidhiana Ardhi zilizotengwa kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya Bandari Kavu katika nchi hizo ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa mkakati wa kukuza biashara.
Akizungumza katika tukio hilo mjini LUBUMBASHI nchini DRC, katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara amesema kuwa hatua hiyo ni matokeo muhimu katika kutekeleza makubaliano ya uendelezaji wa miundombinu ya Uchukuzi yalisainiwa mwaka 2022 ili kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili pamoja na kuboresha mazingira ya usafirishaji mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Baada ya kukamilishwa kwa mazungumzo hayo, Pande zote mbili zinaendelea na ukamilishaji wa taratibu za umilikishwaji wa Ardhi kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa Bandari kavu ambapo kwa DRC, Tanzania itapewa maeneo ya Kasumbalesa, Kasenga na Kalemie huku kwa upande wa Tanzania, DRC itapewa maeneo ya Bandari kavu katika eneo la Kwala Mkoani Pwani na Katosho Mkoani Kigoma.
DRC moja ya masoko yenye wateja wakubwa wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam na Tanga kusafirisha mizigo ya aina mbalimbali inayotoka na kuingia nchini DRC.
Tanzania na DRC ni miongoni mwa nchi Saba zilizopo katika ushoroba wa kati (central corridor) ambapo lengo lake kuu ni kurahisisha usafirishaji kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, reli, usafiri wa majini pamoja na anga.