Select your language

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inashiriki katika maonesho ya Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Ziwa Tanganyika (Lake Tanganyika Business and Investment Forum) linalofanyika mkoani Kigoma.

 

TPA Kupitia jukwaa hilo, inatoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu huduma za bandari, fursa za uwekezaji katika miundombinu ya bandari, pamoja na nafasi ya bandari katika kurahisisha biashara ya kikanda.

 

Kongamano hilo limefunguliwa rasmi Aprili 16,2026 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye katika hotuba yake amesema kuwa jukwaa hilo ni fursa muhimu ya kufungua milango mipya ya ushirikiano wa kiuchumi, kuvutia uwekezaji, na kuimarisha maendeleo endelevu katika ukanda wa Ziwa Tanganyika kwa kuzingatia matumizi bora ya rasilimali na kukuza biashara baina ya nchi wanachama.

 

Katika kongamano hilo, TPA inashiriki kikamilifu kwa kuwa na banda la maonesho pamoja na uwakilishi ndani ya majadiliano, ikitoa elimu kwa wadau kuhusu majukumu yake ya kusimamia na kuendeleza bandari nchini, miradi ya maboresho ya bandari katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, pamoja na mikakati ya kuongeza ufanisi wa Bandari zake.

 

Ushiriki wa TPA katika jukwaa hilo ni hatua muhimu katika kuimarisha nafasi ya bandari kama mhimili wa biashara na uchumi wa kikanda. Kupitia ushiriki huu, TPA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha huduma za bandari na kukuza biashara kati ya nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika.

 

Kongamano hilo linawakutanisha viongozi wa serikali, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika, zikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mwenyeji.