TPA YASHIRIKI ZOEZI LA UOKOAJI KWA WAATHIRIKA WA GHOROFA LILILOPOROMOKA KARIAKOO

Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeshiriki katika zoezi la uokoaji wa wathirika wa ajali ya Ghorofa liliroporomoka katika kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vya uokoaji.
TPA imetoa msaada wa vifaa vya uokoaji kama kofia ngumu, vizibao, glovu, na mtambo maalum wa kunyanyua vitu vizito ili kusaidia kazi za uokoaji zinazoendelea katika ajali hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, wakati wa kukabidhi vifaa mbalimbali vya uokoaji katika eneo la tukio, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus, alisema TPA imesikitishwa sana na tukio hilo lililosababisha vifo na majeruhi, na kuwaombea waliopatwa na mkasa huo wapate uponyaji wa haraka.
“TPA, kama wadau wakubwa wa biashara na wafanyabiashara wa Kariakoo na Tanzania kwa ujumla, tumeguswa sana na tukio hili kwa sababu waathirika ni wadau wetu na Watanzania wenzetu,” alisema Bw. Gallus.