Select your language

Watumishi wanawake wa Bandari za Ziwa Victoria wakiongozwa na Meneja wa Bandari, Bi. Rosemary Ndesamburo, wameungana na wanawake wengine wa Mkoa wa Mwanza kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela, Mkoa wa Mwanza.

 

Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa kauli mbiu ya “Haki ya Wanawake na Wasichana ni Msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira ya 2050” yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, ambapo mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda.

 

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mkuu wa Mkoa aliwahimiza wanawake kuendelea kujijenga kiuchumi na kijamii kwa kufanya kazi kwa bidii, kujithamini na kujiandaa vyema kwa maisha yao ya baadaye, hususani kipindi cha uzeeni. Aidha, aliwasisitiza wanawake kuendelea kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kupanda miti na kutunza rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

Kwa upande wao, watumishi wanawake wa Bandari za Ziwa Victoria walieleza kuwa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni fursa muhimu ya kuendelea kuhamasisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na mchango wao katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

 

Menejimenti ya Bandari za Ziwa Victoria inaendelea kuthamini na kuunga mkono juhudi za kuwawezesha wanawake katika maeneo ya kazi na katika jamii, kwa kutambua kuwa wanawake ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu ya Taifa