Select your language

Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani, Wanawake watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania( TPA) ,tarehe 12 Machi 2025, wameshiriki matendo ya huruma kwa kutoa misaada ya vifaa tiba katika hospitali za Wilaya ya Kigamboni na Temeke vyenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 49.

Akipokea vifaa tiba hivyo vya aina 15 tofauti, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe.Halima Bulembo amesema hii si mara ya kwanza kwa TPA kutoa misaada katika Wilaya hiyo,na kwa kitendo hicho anaishukuru sana Menejimenti ya TPA.

Akizungumza wakati anakabidhi vifaa tiba hivyo.Meneja Rasilimali Watu wa Bandari ya Dar es Salaam Bi.Mwajuma Mkonga, amesema TPA imetoa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 24 katika hospitali ya Kigamboni na katika hospitali ya Rufaa ya Temeke wametoa vyenye thamani ya shilingi milioni 25.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Daktari Bingwa wa macho Annamary Rugakiza Stanslaus, ameishukuru TPA hususani Wafanyakazi wanawake kwa msaada wao ambao utaenda kuwasaidia kwa kuokoa maisha ya wakinamama na watoto wachanga.