WATUMISHI WANAWAKE WA BANDARI YA TANGA WASHIRIKI MATENDO YA HURUMA
Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2026 Watumishi Wanawake wa Bandari ya Tanga waliungana na Wafanyakazi Wanawake wa kutwa wa bandari hiyo kufanya matendo ya huruma.
Wanawake hao, walitoa msaada wa Mashine za kusaidia upumuaji aina ya “C- PAP Bubble Neonates, Oxygen Flowmeter” pamoja na vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo vyenye thamani ya Shilingi Milioni 5.
Akizungumza wakati wa kukabidhi Mashine hizo, Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Bandari hiyo, Bi. Sharifa Nuhu alisema, wamekuwa na utaratibu wa kila mwaka kutumia siku hiyo kufanya matendo ya huruma kwa jamii na mwaka huu wasaidie Hospital ya Rufaa ya Mkoa, Bombo.
“ Mwaka huu tumeona tuunge mkono juhudi za Serikali katika kuboresha afya za watoto, hivyo tukaona tutoe msaada wa Mashine hizo katika wodi ya watoto wachanga katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo sababu ndio hospitali kubwa ambayo hata wagonjwa kutoka hospitali za Wilaya hupewa rufaa ya kuja hapa kufanya uchunguzi zaidi wa kitabibu”. Aliongeza Bi. Nuhu.
Awali akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa, Dkt . Abdi Msangi aliwashukuru Watumishi hao kwa msaada walioutoa kwani umetolewa wakati muafaka kutokana na uwepo wa upungufu wa mashine hizo katika wodi ya watoto wachanga wenye matatizo ya upumuaji.
Aidha Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali hiyo, Dkt. Mohamed Salehe alisema kuwa Mashine hizo zitakuwa msaada mkubwa hospitalini hapo ikizingatiwa kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wanaozaliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na shida ya upumuaji. Kwa hiyo vifaa hivyo vitaenda kuboresha huduma ya upatikanaji wa huduma katika wodi ya watoto.

”
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"