Select your language

Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uboreshaji na uendeshaji wa bandari nchini, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa huduma za bandari na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), tarehe 9 Februari, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo alipata fursa ya kukagua maendeleo ya miundombinu na utendaji wa shughuli mbalimbali za bandari.

Profesa Mbarawa amesema kuwa Serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kuboresha miundombinu ya bandari, ikiwemo kuimarisha huduma za upakiaji na upakuaji mizigo, kupanua na kuboresha magati, pamoja na kuvutia uwekezaji zaidi wa kimkakati katika sekta ya bandari.

Aidha, Mhe. Waziri amebainisha kuwa ushirikiano huo una lengo la kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za biashara, na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika kukuza uchumi wa taifa.

Mapema Mhe. Waziri Prof. Mbarawa alipewa maelezo ya kina ya kiutendaji na shughuli za utekelezaji katika Bandari ya Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mha. Dkt. Baraka Mdima kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa.