Select your language

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) kwa usimamizi mzuri wa matumizi ya Fedha za Maboresho yanayoendelea kufanyika kupitia mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP)

Akizugumza tarehe 30 Machi 2025, mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua na kutembelea mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, Mwenyekiti wa PAC , Mhe.Naghenjwa Kaboyoka (Mb) amesema kamati yake imejiridhisha na usimamizi mzuri wa Mradi huo na Fedha za Umma zimetumika vyema na kufikia malengo yakiyokusudiwa.

“ Kamati imejiridhisha na kazi nzuri iliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, kazi yetu kubwa ni kuangalia Kama Fedha za Umma zimetumika vizuri kwa manufaa ya nchi yetu na katika hili Kamati inampongeza sana Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti ya TPA na Wafanyakazi wote kwa kazi nzuri iliyofanyika hapa.’ Amesema Mhe. Kaboyoka.

Akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Mhe. Balozi na IGP Mstaafu Ernest Mangu, ameishukuru Kamati kwa kufanya ziara yao iliyowawezesha kuona hatua iliyofikiwa na thamani ya mradi wa DMGP, huku akiihakikishia kamati hiyo kuwa maelekezo, maoni na ushauri wao utafanyiwa kazi.

Mapema akisoma taarifa ya mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) mbele ya kamati kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mbossa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka Mdima, amesema hadi sasa kukamilika kwa utekelezaji wa mradi katika baadhi ya maeneo kumeleta manufaa mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia Meli kubwa zenye kubeba makasha hadi 8,000, kuongezeka uwezo wa kuhudumia shehena kutoka tani milioni 16 hadi tani milioni 28 kwa sasa na kuongeza uwezo wa kiushindani kati ya Bandari ya Dar es Salaam na Bandari nyingine.

Mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) unagharimu Shilingi Trilioni 1.118 ambazo ni Fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia, Fedha za msaada kutoka kwa Wafadhili na mapato ya ndani ya TPA.

Mradi huu umehusisha kuimarisha Gati na 1-7 na kuongeza kina kutoka mita 8 hadi mita 14.5 na kujenga Gati maalum ( RoRo Berth) la kuhudumia meli za magari, kuongeza kina na Upana wa lango la kuingilia Meli na eneo la kugeuzia Meli , kuimarisha Gati na 8-11 na kuongeza kina kutoka mita 12 hadi kufikia kina cha mita 14.5, kuboresha mtandao wa Reli ndani ya Bandari na kusimika Mfumo wa Umeme Bandarini.