TPA YASHIRIKI KONGAMANO LATATU LA UCHUKUZI NA BIASHARA (LAND-LINKED ZAMBIA TRANSPORT ANDLOGISTICS EVENT)

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kongamano la tatu la Uchukuzi na Biashara (Land-Linked Zambia Transport and Logistics event) lililofanyika Jijini Lusaka kuanzia tarehe 4 hadi 5 Aprili, 2024, limeiwezesha Tanzania kutangaza maboresho makubwa yanayofanyika katika sekta ya miundombinu wezeshi nchini ili kuchochea uchumi Zambia na nchi nyingine zinazohudumiwa na Bandari za Tanzania.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa katika Kongamano hilo na Balozi wa Tanzania nchini Zambia Luteni Jenerali Mathew Mkingule, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi Mhe. Profesa Makame Mbarawa, ambapo amesema Kongamano hilo limeiwezesha Serikali kuelezea kuhusu maboresho makubwa yaliyofanyika katika miundombinu kwenye sekta ya Uchukuzi ikiwemo Bandari zake zinazohudumia nchi mbalimbali ikiwemo Zambia.
TPA imeshiriki kongamano hilo la siku mbili likihusisha Taasisi za sekta ya uchukuzi kwa ukanda wa Nchi za kusini mwa Afrika kama Mdau na mmoja wa wadhamini Wakuu.