Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhandisi Cyprian Luhemeja, ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kuendelea kutangaza huduma zake na kuwafikia wateja kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 98 ya Kilimo na Biashara (98th Agriculture and Commercial Show) yanayoendelea jijini Lusaka.
Balozi Luhemeja alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la Tanzania katika maonesho hayo, akieleza kuwa ushiriki wa TPA ni hatua muhimu ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Zambia pamoja na kuongeza matumizi ya Bandari za Tanzania kwa wafanyabiashara wa Zambia na nchi jirani.
Maonesho hayo yamefanyika kuanzia Julai 29,2026 na yatafungwa Agosti 3, 2026, yakikusanya washiriki kutoka sekta mbalimbali za biashara na kilimo ndani na nje ya Zambia. Kupitia maonesho hayo, TPA imekuwa ikitoa elimu kuhusu huduma za bandari, maboresho ya miundombinu na fursa zinazopatikana katika Bandari za Tanzania, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kusogeza huduma karibu na wateja na kuimarisha biashara ya kikanda.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Balozi Luhemeja alisema TPA imeonyesha dhamira ya dhati ya kuwahudumia wateja kwa ufanisi kwa kuwafuata walipo, jambo linalochangia kuongeza ushindani wa Bandari za Tanzania na kuimarisha nafasi yake kama lango kuu la biashara kwa nchi zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam.
Mbali na TPA, taasisi nyingine za Tanzania zilizoshiriki katika maonesho hayo ni pamoja na ATCL, MOI, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya pamoja na wajasiriamali wadogo waliowasilisha bidhaa na huduma mbalimbali zinazotangaza uwezo na fursa za Tanzania.
Ushiriki wa TPA katika Maonesho ya 98 ya Kilimo na Biashara nchini Zambia unaakisi dhamira ya Mamlaka ya kuendelea kupanua masoko, kuimarisha uhusiano na wadau wa biashara wa kikanda na kuhakikisha wateja wanapata huduma bora zinazokidhi mahitaji yao.