Bandari ya Dar es Salaam imeandika rekodi mpya kufuatia kuhudumia jumla ya Tani Milioni 33.7 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 . Kiwango hicho ni sawa na ongezeko la Tani Milioni 6 ikilinganishwa na jumla ya Tani Milioni 27.7 zilizohudumiwa Mwaka wa fedha 2024/2025. Kufuatia mafanikio hayo Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed amewapongeza wafanyakazi wa Bandari hiyo tarehe 15 wakati akifungua Kikao cha 3 cha Baraza la Majadiliano (JIC) cha Bandari ya Dar es Salaam kinachofanyika mjini Bagamoyo. 

Bw. Gallus ametaja sababu za ongezeko hilo ikiwa ni pamoja na maamuzi dhabiti ya Serikali ya kuweka taasisi binafsi ambayo yamefanya mapinduzi makubwa katika huduma za kibandari na kusababisha rekodi hiyo iliyotazamiwa kufikiwa mwaka 2030. Amefafanua kwamba, awali tofauti ya kuhudumia shehena kwa kila mwaka ilikuwa ni Tani milioni 1 hadi Tani milioni 1.5 lakini tangu uwekezaji kufanyika kumekuwa na ongezeko kubwa ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 tofauti ilikuwa ya Tani Mil. 4 lakini kwa mwaka 2025/2026 imeongezeka kufikia Tani Mil. 6

Amesema ongezeko hilo la kila mwaka limethibitisha umuhimu wa uwekezaji wa taasisi binafsi ambapo kwa matokeo hayo chanya wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wanaidhihirishia Serikali kwamba maamuzi yaliyofanywa yalikuwa sahihi. Pamoja na mambo mengine Baraza hilo limewataka Wafanyakazi kujitokeza katika Kituo cha Afya cha Bandari ya Dar es Salaam (PHC) kwa ajilli ya kupima afya zao ili kutambua mapema viashiria vya magonjwa sugu yasiyoambukiza kwa lengo la kuwa na wafanyakazi wenye afya njema watakaopelekea kuongezeka kwa ufanisi zaidi. Baraza la Majadiliano (JIC) linaloendelea litajadili taarifa ya utekelezaji wa Makubaliano yatokanayo na Kikao Namba 2 cha Mwaka 2025/2026 kilichofanyika tarehe 17 na 18 Machi 2026 mjini Bagamoyo.